KUSANYIKO KUU LA TISA EFATHA MINISTRY PRECIOUS CENTER KIBAHA:
NENO NA: DR. MORRIS CERULLO KUTOKA US:
Tanzania ni Mali ya Bwana Yesu:
Tarehe 2/10/2017 ilikuwa ni siku yangu ya kuzaliwa, nilikuwa natimiza miaka 86. Miaka 71 katika Huduma na miaka 66 ndani ya ndoa.
Mimi nilikuwa ni kijana ambaye sina wazazi yaani (yatima). Nilimpoteza Mama yangu nikiwa na miaka miwili na Baba yangu alikuwa ni mlevi sana hivyo asingeweza kunisaidia. Serikali ya jimbo tulilokuwa tunaishi ikaichukua familia yangu na mimi nikalelewa katika kituo cha watoto yatima.
Nilipotimiza umri wa miaka 15 nilimuomba Mungu, huyu Mungu wa Musa, Ibrahimu , Yakobo, Yoshua na Eliya akaja kwangu niliyekuwa yatima mdogo nikiwa na umri wa miaka 15 na akanileta kwa Yesu.
Katika umri huo ndipo Mungu akanitoa katika kituo cha watoto yatima, akanichukua na kunipeleka Mbinguni na kwa macho yangu niliuona Utukufu ule ule wa Mungu ambao Musa aliuona. Baada ya yale maono nikatoa maisha yangu yote kwa Mungu. Kwa miaka 71 sijawahi kurudi nyuma katika kumtumikia Mungu wangu.
Mwaka mmoja uliopita nilikuwa naelekea kufa kutokana na ugonjwa wa Vascular niliokuwa nao. Nilikuwa mgonjwa sana na sikuweza hata kutembea kwani mguu wangu mmoja ulikuwa umelika sana nikawa nime pooza mguu huo mmoja. Ugonjwa huu unakula nyama na hata mifupa. Hakukuwa na dawa ya kuweza kunitibu nikawa natumia vidonge vya kupunguza maumivu tu, kwani maumivu yalikuwa ni makali sana saa 24, yalikuwa ni maumivu ya kutisha.
Nilipokuwa mgonjwa sikujiombea mimi mwenyewe, bali watu waliokuwepo Tanzania na Dunia yote waliomba kwa ajili yangu na mimi nikaomba. Lakini ombi langu lilikuwa ni la tofauti na wengine. Mimi nilikuwa namuomba Mungu anichukue nikapumzike kwani nilimpa miaka 71 katika maisha yangu katika kumtumikia yeye, hivyo nilikuwa natamani kwenda kwake, sikutamani kuishi tena. Nikamwambia Mungu nimekupa miaka 71 unataka nini cha zaidi?
Mimi nina mke ni muombaji wa ajabu, akaniambia Mume ni kichwa cha familia, ni sawa kabisa lakini mke ni shingo ambaye anakigeuza geuza kichwa hivyo mwanamume hawezi kuishi bila mke.
Wakati mimi ninamuomba Baba anipeleke nyumbani yaani (Mbinguni), mke wangu naye akawa anaomba kwa Mungu asinichukue kwa sababu bado sijamaliza kazi ya Mungu kwani kuna vitu vingine anataka nifanye, hivyo asinichukue.
Siku moja nikiwa nimeketi katika kiti changu cha kubebea wagonjwa (wheel-chair) nikiwa siwezi kutembea nikawa naomba. Wakati nikiwa naomba nilishangaa kukawa na uwepo wa ajabu sana katika kile chumba nilichokuwepo ulikuja na kuniingia katika mwili wangu nikashangaa sana, nikaamka na kuanza kuruka ruka, nikapokea uponyaji wangu saa ile ile. Na sasa Mungu amenipa ngozi mpya katika mguu wangu. Kweli huu ni muujiza wa ajabu sana namshukuru sana Mungu kwa matendo yake ya ajabu kwangu.
Mimi kuwepo Tanzania leo si kwa bahati mbaya bali Mungu alinituma kwa ajili ya Tanzania. Ninaenda kumuomba Mungu aachilie Upako mpya katika maisha yako, nguvu ile ile ambayo iliniponya mimi, leo hii ikakuponye na wewe na kubadilishe maisha yako pia, katika Jina la Yesu.
Mimi na Mke wangu, huwa tuna kitu kidogo cha kufanya kabla ya kulala kila siku usiku. Huwa tunashikana mikono kwa ajili ya kuiombea Dunia yote na kuiombea Tanzania kila usiku. Tunamuomba Mungu akawape mpenyo na kuzilinda familia zenu pia. AMEN.
Tanzania ni mali ya Yesu.

Comments