SEHEMU YA MAHUBIRI YA IBADA YA JUMAPILI 9 March 2014

Mtumishi wa MUNGU Mkalimani wetu Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira, EFATHA MINISTRY.

"Katika Agano la MUNGU kwetu Mwaka huu amesema ni mwaka wa KIBALI, utaenda kuuona ukuu wa MUNGU, Mwanzo: 12:1-3 (BWANA Akamwambia Abramu …) MUNGU Anaongea na mtu wake “Toka”, na sio watu ila wewe. Ili uweze kuelewa ujumbe wa Kibali fanya KIBALI chako kiwe cha binafsi, Usifanye cha harambee, Kibali chako ni cha kipekee.

Kumbuka kuna mtu anashuhudia matendo makuu ya MUNGU aliyomtendea kila iitwapo leo maana yake amemfanya MUNGU kuwa ni wa kwake lakini wewe tangu ushuhudie mwaka juzi hujashuhudia tena, MFANYE MUNGU WA Kwako.

TOKA;
- Toka wewe katika Nchi yako - kuna tabia za kitaifa/ tabia za nchi zisizofaa, Toka katika hizo.
- Toka wewe katika jamaa zako - kuna tabia za jamii/ unawafahamu huko toka, TOKA katika tabia mbaya za jamaa zako unaowafahamu, wanaokuzunguka.
- Toka wewe katika nyumba ya baba yako – toka katika tabia za nyumba ya baba yako.

Kwa hiyo sisi hatuna haja ya kutoka nchini kwetu na kwenda ulaya kutumikishwa hiyo siyo akili nzuri. Walokole wengi wameokoka lakini “Kutoka” katika tabia za baba zao, nchi yako, jamaa yako bado hawajatoka, hilo ni tatizo, Bibilia inasema katika kitabu cha Amosi ‘Niondoleeni kelele zenu’ ni kweli unaweza kufunga kwalezima/ ramadhani, Bibilia inauliza ‘hiyo ndiyo saumu niliyokueleza’? Siku UTAKAPOTOKA katika TABIA za nchi yako, jamaa zako, Uzao wa baba yako nakuhakikishia MUNGU Atakuonyesha NJIA ya kwenda. Unapoamua KUACHANA na Tabia za nyumba ya baba yako, Jamaa zako, Nchi yako UTUKUFU WA MUNGU Utakuzunguka.

Mnasikia sana Mafundisho, Mahubiri lakini kuchukua hatua ya kutenda inakuwa kazi, nakumbuka mimi nilipoamua kutoka katika tabia za nchi yangu, jamaa zangu, na katika tabia za nyumba ya baba yangu, nilibaki peke yangu hata wale niliokuwa nasali nao walisema usifuatane na sisi wenye dhambi. Unapoamua kuachana na dhambi UTUKUFU WA MUNGU Unakufunika, hata nilipokuwa nasali KKKT nikisimama kuhubiri kweli ya MUNGU wazee wa kanisa wananitoa nje, maana walikuwa hawataki kunisikiliza niwaambie kile NINACHOELEKEZWA na MUNGU.

IBADA maana yake nini?, Ibada maana yake ni watu kupeleka MAHITAJI yao kwa MUNGU na MUNGU kuwajibu, Ibada sio Utakatifu, MUNGU hufanya mambo yake kwa sekunde chache inategemea ulivyojiandaa. Kutoka kuna gharama, MUNGU alimuambia “Toka” katika nyumba ya baba yako, Ibrahimu alipotoka akakosea akatoka na baba yake, lakini baba yake alifia njiani maana MUNGU haitaji mizigo!

TOKA; Ukishatoka ndio Anakuonyesha, ni kweli “Amekuokoa, Amekufungua, Amekuweka HURU”, lakini Anataka UTOKE."



Comments