MANENO YENYE HEKIMA NA UFAHAMU: (Mkalimani Mtumishi wa MUNGU Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira).

''Watu wengi wameumizwa na marafiki wa karibu kwa sababu hawakujua wanawawazia nini kila siku. Tunashuhudia Serikali zikipinduliwa na Marafiki miongoni mwa kundi hilo hilo, pia Mauaji ya halaiki yakifanywa na watu wanaofahamiana, kwa sababu Moyo wa Mwanadamu ni mdanganyifu. Siyo rahisi kufahamu anachowaza wakati wowote. Tunasoma, “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; Nani Awezaye kuujua?” (Yeremia 17:9). Moyo hubadilika kila wakati kutegemeana na mazingira na mazoea ya mtu aliyojijengea. Wapendanao wanaweza kufarakana vikali na chuki ya kutisha kuibuka kwa sababu ya moyo!. Mtu bila KUJIJUA, anaweza kuwa na Kijicho, Hila, Matusi, Ukorofi, Kiburi, Upumbavu n.k. mambo ambayo ni MATUNDA ya Moyo. Ndani ya moyo wa Mtu hutoka Mawazo mabaya, Uasherati, Wivu, Uuaji, Uzinzi, Husuda na Kadhalika. Maovu haya yote yanamtia mtu Unajisi, ni VIZURI KUYASHUGHULIKIA. Biblia inasema; “Akasema, kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi” (Marko 7:20 -23). Pia ndani ya Moyo panaweza kuzaliwa “TUNDA LA ROHO ambalo ni Upendo, Furaha, Amani, Uvumilivu, Utu wema, Fadhili, Uaminifu, Upole Kiasi,” (Wagalatia 5: 22-23)
Mfano: Nyakati za BWANA Wetu YESU KRISTO, baadhi ya Wanafunzi wake wa karibu kabisa walikuwa wakiwaza mambo asiyodhania, japokuwa BWANA YESU ALIWEZA kupambanua mawazo ya Mioyo ya watu. Wengine waliwaza juu ya nafsi zao katika kundi kuliko kuwaza jinsi ya kudumisha Huduma ya BWANA wao, na wengine walifika mbali zaidi hata Kumsaliti kwa fedha. Pia nyakati za Matendo ya Mitume baadhi ya watu waliookoka, wapo waliotamani vipawa vya ROHO MTAKATIFU kiasi cha Kutaka Kutoa RUSHWA, mfano Simion (Matendo 8: 18-24) Ukifuatilia mfululizo wa Safari ya Huduma ya BWANA YESU hapa duniani, Utabaini kuwepo kwa Vituko vya aina aina vinavyoonyesha Moyo wa MTU ULIVYO WA KUSHANGAZA. Ndiyo Maana ni MUHIMU SANA MTU KULINDA MOYO WAKE Kuliko Vitu Vyote.''

Comments