SOMO: ROHO SABA ZA MUNGU.

Zakaria 4:6 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi. ”

Kuna mambo matano ambayo Roho Saba zimebeba nayo ni:-
1. Upendo wa Mungu; Upendo ni kama chombo ambacho kinabeba Roho wa Mungu na ndio maana Biblia inasema “Mungu ni Pendo.”
Wokovu ni Roho lakini haiwezi kwenda kwa mtu bila Upendo wa Mungu, kwa maana Biblia inasema “kwa jinsi hii Mungu aliupenda Ulimwengu hata akamtuma mwanae wa pekee” Hivyo ina maana kuwa Roho hizi Saba zimebeba Upendo wa Mungu.

2. Neema yake; Neema imebeba msamaha kama huna Neema huna MSAMAHA wala REHEMA bali una HUKUMU.
NEEMA inabeba REHEMA za Mungu, HURUMA na MSAMAHA wa Mungu. Yeyote asiyeweza KUSAMEHE ina maana kuwa yeye mwenyewe hajasamehewa, Wokovu ni Neema, Kama Neema haipo kwa mtu ina maana Wokovu haupo.

Bila Neema kamwe hutaweza kuwa MTII, na hata kama ukiwa unajua umekosea bado utaendelea kuwa mbishi kwa sababu huna Neema hivyo hujasamehewa na Mungu. Mtu yeyote anayeweza kusamehe wengine amesamehewa.

Kuipata Neema si jambo rahisi kama unavyo fikiri maana mara zote ndani ya Neema kuna maumivu makali sana ndipo tunaitaji UTII.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba. Mungu ana Upendo, anasamehe, anapo kusamehe ina maana kuwa unapokea Neema ambayo ni Wokovu.
Bwana Yesu alipokuja aliibeba NEEMA, MSAMAHA WA DHAMBI, HURUMA na REHEMA za Mungu na ndio maana alikwenda msalabani, Neema ina maumivu. Warumi 12:1 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. ”

Neema ina maana gani? Ni UTII kwa Mungu. Haikuwa rahisi kwa Yesu kufa msalabani lakini kwa sababu ya NEEMA akatimiza mapenzi ya Mungu. Mapenzi ya Mungu yapo kwenye Neema unapo tii ina maana kuwa unatimiza Mapenzi ya Mungu.
Ni Neema tu ndiyo itakayo kusababisha wewe ukae katika mstari. Neema tu ndiyo inaweza kutunza Upendo wako kwa Yesu. Nje ya neema hutakaa ufanikiwe, wala hutakaa utembee sawa sawa na wenye haki wa Mungu.

Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira.

Comments